Wednesday 15 January 2014

Kuhusu Tukio la Daladala Mbili kuteketea Kwa Moto Mkoani Iringa kwa sababu ya Wanafunzi,Ingia hapa

Wananchi wa Iringa mjini wakilitazama daladala lililowaka moto wakati likiwa kwa mafundi wa kuchomelea leo eneo la uwanja wa Samora mkoani Iringa.
Konda wa daladala hilo akiwa na kifaa cha kuzimia moto ambacho kimenusurika katika moto huo.
Askari wa Kikosi cha Zimamoto Iringa mjini wakilitazama daladala hilo.
Muonekano wa ndani wa daladala hiyo baada ya kuwaka moto.
Hili ni basi ambalo pia limeungua upande wa mbele.
Askari wa Kikosi cha Zimamoto na uokoaji Iringa mjini Bw. John Zacharia akikagua kifaa cha kuzimia moto ambacho kilikutwa kikiwa kibovu.

BASI moja lImenusurika  kuwaka wakati daladala moja  ikiteketea yote kwa moto wakati  wanafunzi wa masomo ya  kuunga vyuma katika gereji  bubu eneo la uwanja  wa  Samora  mjini  Iringa  wakijifunza kuunga ngao ya daladala hiyo yenye  namba za usajili T189 AWN.

Tukio  hilo  limetokea  leo majira ya 8:15 mchana wakati vijana wawili wanaojifunza kuunga wakiendelea na mafunzo ya kuunga ngao ya daladala  hiyo.

Akizungumzia ajali hiyo mmoja kati ya wafanyakazi wa gereji  hiyo, Filibert Mwihava alisema kuwa chanzo cha daladala hiyo kuwaka moto ni vijana wawili ambao  wanajifunza ufundi wa kuunga vyuma katika eneo hilo kufanya kazi hiyo bila kuzingatia kanuni ya kazi hiyo.

Kwani  alisema vijana hao walikuwa wakiunga ngao ya nyuma ya daladala  hiyo jirani na tenki la mafuta na kutokana na cheche zilizokuwa zikitoka zilisababisha moto kuibuka kwa kasi.

Hata hivyo alisema mbali ya kuwa na kifaa cha kuzimia moto bado walishindwa kukitumia kifaa hicho kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha ya kukitumia.

Mwihava alisema kutokana na moto huo kushika daladala hiyo inayofanya  safari  zake kati ya Tumaini na Zizi la Ng'ombe mjini Iringa hakuna mtu aliyezulika zaidi ya basi  lenye namba za usajili T 457 AMQ kuungua upande wa mbele kabla ya kuokolewa.

Pia alishukuru askari wa Kikosi cha Zimamoto na uokoaji mjini Iringa ambao walifika kwa wakati na kufanikiwa kuzima moto huo ambao ungeweza kusababisha madhara  makubwa katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na ofisi na maduka ya watu waliojenga kuzunguka uwanja wa Samora kuteketea.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kiongozi wa askari wa Kikosi cha Zimamoto ambao walifika eneo hilo John Zacharia alisema kuwa chanzo cha moto huo ni uzembe wa ofisi hiyo.

Kwani alisema hata kifaa cha zimamoto  walichokuwa nacho kilikuwa hakifanyi kazi kutokana na kuharibika muda mrefu.

Zacharia aliwataka wamiliki wa vyombo vya usafiri kuzingatia sheria za zimamoto ya kuwa na vifaa vya kuzimia moto badala ya kudanganya na kuona kama wanaonewa  pale wanapolazimishwa kuwa na vifaa hivyo

No comments:

Post a Comment