Thursday, 7 August 2014

John Mnyika- Katiba Mpya ni vigumu kupatikani mwaka huu 2014



Mbunge wa jimbo la Ubungo Mh.John Mnyika amefunguka na kuweka wazi kuwa Katiba Mpya haiwezi kupatikana mwaka 2014 kama ambavyo ilikuwa ikitarajiwa,Mnyika amefunguka hayo leo akiwa katika kipengele cha Kikaangoni Live

Mbunge wa jimbo la Ubungo Mh.John Mnyika alipokuwa akichat Live leo katika ukurasa wa Facebook wa EATV.
kinachofanyika kila siku ya Jumatano kupitia ukurasa wa Facebook wa EATV.
Mnyika amesema kuwa hata kama ikitokea UKAWA wakirudi bungeni suala la kupatikana kwa katiba mpya litakuwa ni kitendawili kutokana na namna mchakato ambao ni lazima kupitia ili kupata hiyo Katiba mpya.
"Ni kweli 2014 haiwezekani kupatikana kwa Katiba mpya,kwani siku 60 alizotoa Rais Kikwete hata kama UKAWA ikirudi bungeni hazitoshi kumaliza ibara zote 271 na sura 17 kama mpaka sasa zinabishaniwa sura mbili tu. Hata kama ikipatikana, itahitaji kupigiwa kura ya maoni, kwa taarifa nilizonazo toka ndani ya tume ni kwamba inawezekana ikiwa Mwezi Machi 2015.Hata ikiwa muda huo, Shirikisho la Serikali Tatu likiwa ndio muundo Katiba za Tanganyika na Zanzibar zitapaswa kuandikwa upya. Hivyo, kutahitajika Bunge Maalum na kura ya maoni ya Tanganyika, na hata tume ya maoni hata kama itatumia maoni kwa sehemu yaliyokusanywa na Warioba na rasimu ambayo wanadai wanayotayari. Hata kama ingekuwa katiba mpya ya Serikali mbili, bado Sheria muhimu zinazokinzana na katiba mpya zitapaswa kuandikwa upya. Hivyo, kwa vyovyote vile, katiba mpya haiwezi kutumika kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Mbali na hilo Mnyika ameweka wazi msimamo wa Umoja wa Katiba ya Wanchi (UKAWA) kuwa hawawezi kurudi katika Bunge Maalumu la Katiba kama hakutakuwa na maridhiano yenye kuheshimu na kutambua maoni ya wananchi na kutambua misingi ya rasimu ya Katiba uliyotokana na maoni ya wananchi.
"Mwezi ujao hatutaingia, labda kuwe na maridhiano yenye kuheshimu maoni ya wananchi, kuheshimu misingi muhimu ya rasimu iliyotokana na maoni ya wananchi na kuwa na tafsiri sahihi yenye mipaka kuhusu mamlaka ya Bunge hilo. Nini kitatokea, Bunge Maalum haliwezi kuendelea ama litakosa theluthi mbili (2/3) ya kuweza kupitisha hiyo rasimu kwa mujibu wa sheria au hata kukifanyika ufisadi wa kurubuni baadhi ya wajumbe maamuzi ya Bunge hilo yatakuwa hayana uhalali wa kukubalika (illegitimate).
Katiba ni muafaka wa kitaifa, kama muafaka usipokuwepo; mchakato wa katiba utakwama na katiba hiyo itakataliwa na wananchi kwenye kura ya maoni. Hivyo, kuepusha kuendelea kutumia vibaya fedha za Umma kama ilivyotokea katika mkutano uliopita wa Bunge Maalum, Mkutano ujao usianze mpaka kwanza maridhiano yaweze kufikiwa nje ya Bunge."
TATIZO LA MAJI UBUNGO
Tatizo la maji katika jimbo la ubungo imeonekana ni tatizo kubwa linalosababisha watu mbalimbali kuichukia serikali na viongozi wake kwa kushindwa kutatua tatizo hilo ambalo limekuwepo kwa muda mrefu sasa,lakini mbunge wa jimbo hilo la ubungo anaweka wazi namna gani ambavyo amekuwa akijitahidi kuishauri serikali.
"kazi ya Mbunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali. Hii ni kwa mujibu wa mamlaka na madaraka ya Bunge ya Ibara ya 63, nimeifanya kazi hiyo kwa njia mbalimbali- kuna maeneo tumefanikiwa yanapata maji na kuna maeneo bado ndio maana naendelea kuisimamia Serikali ili ufumbuzi upatikane kwa haraka zaidi. Hata hivyo, kwa mujibu wa tafiti mbalimbali matatizo ya maji ndio kero namba moja sio kwa Ubungo tyu bali kwa maeneo mengi nchini. Ndio maana mkutano uliopita wa wabunge niliotoa hoja wakati wa bajeti ya Wizara ya Maji ya kushikilia shilingi kwenye mshahara wa Waziri juu ya mpango wa maji nchi nzima ambayo kwa kiasi iliungwa mkono, nitaifuatilia kwa karibu zaidi utekelezaji wake katika mkutano wa Bunge mwezi Novemba 2014. Kabla ya Mkutano huo, naendelea kufuatilia wiki ofisi ya Rais ili akirejea ziarani kile kikao alichoahidi ikulu kifanyike utekelezaji wa miradi uharakishwe."
URAIS SIO KITU RAHISI SIWEZI KUGOMBEA
Mnyika ameonesha wazi kuwa kazi ya kuongoza nchi si kazi rahisi kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakidhania na kuchukulia ndio maana anoanesha wasi kuwa kuna baadhi ya watu wameifanya taasisis hiyo ya Urahisi kuonekana ni kitu chepesi hivyo ndio maana kuwekuwa na watu wengi wamekuwa wakihisi na kuona wanauwezo wa kuongoza nchi na kujiona wana sifa hizo,lakini kwake yeye ameona ni kazi ngumu sana ambayo hawezi kuifanya kwa wakati huu.
"Nishukuru wote wazee, wanawake na vijana ambao kwa nyakati mbalimbali mmenihoji suala hili na wengine kutoa maoni kwamba nijiandae kugombea urais. Urais sio kitu rahisi, ukiangalia kwa sasa taasisi ya urais ilivyofanywa rahisi kutokana na udhaifu uliopo ni wazi wengi wataona kwamba wana sifa za uwezo na uadilifu wa kugombea nafasi hizo; hata hivyo kwa kipindi nilichotumikia wananchi mpaka sasa kama mbunge, na kipindi nilichoshiriki kwenye michakato mbalimbali ya nchi, kimenifanya nibaini kwamba kama kigezo ni kutizama viongozi wa sasa, basi ni rahisi kuwa mpango wa kugombea kuziba ombwe lililopo. Lakini kama kigezo ni uwezo na uadilifu unaohitajika kwa taifa bila kulinganisha na uongozi uliopo bali viwango vya juu vya maono na maadili, basi sina mpango huo kwa sasa.Huu ni wakati wa kutumikia umma katika nafasi ambayo wananchi wameniamini na ni wakati wa kushiriki katika kujenga taasisi mbadala kuwezesha mabadiliko kwa kuwa nchi yetu ina tatizo kubwa la kimfumo ambao nafasi moja tu ya rais haitoshi kutimiza malengo yanayokusudiwa."
WASALITI NDANI YA CHAMA WATACHUKULIWA HATUA
Mnyika ambae ni Mbunge wa Ubungo amesema kuwa viongozi wasaliti katika chama wataendelea kuchukuliwa hatua mbalimbali kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizopo katika chama.
"wasaliti na mamluki katika chama waendelea kuchukuliwa hatua; wengine wanaonywa na wasiojirekekisha wanafukuzwa. Wengine wanachukuliwa hatua ngazi ya taifa wengine ngazi za chini katika maeneo yao. Wasaliti na mamluki hao wengine wameanza kukimbia wenyewe kwa kutambua kwamba wapo walioanza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa katiba, kanuni, maadili na itifaki ya chama na wapo ambao walikuwa wanajua wazi kwamba uchaguzi katika ngazi zao unaoendelea na hivyo kwa umamluki, usaliti au hata walau uzembe wao wa kushindwa kutimiza wajibu katika kipindi kirefu waliochoongoza wanaanza kuondoka wenyewe. Akheri kuwa na nyoka wengi nje ya nyumba kuliko kuwa na nyoka mmoja ndani ya nyuma.Wasaliti na mamluki hao wanatumwa na kutumika tu, hivyo kwa maoni yangu badala ya kushughulika na wasaliti na mamluki hao tu. Nguvu za chama zielekezwe katika kukijenga CHADEMA kama taasisi na pia kukabiliana na hao wanaowatuma na kuwatumia ambao baadhi yao wako kwenye CCM na vyombo vingine vya kiserikali"
SIRI KUONDOA TATIZO LA AJIRA KWA VIJANA.
Imekuwa ikisemwa siku zote kuwa Ajira ni bomu linalosubiri kulipuka kutokana na ukweli kwamba kumekuwepo na vijana wengi nchini wasio na ajira jambo linalopelekea vijana wengi kuwa katika wakati mgumu na maisha magumu.
"Mwaka 2000 niliandika mada "Youth Unemployment: Challenges and Opportunities", mawazo ya wakati ule naamini yanaweza kutumika hata sasa kuondoa tatizo lililopo. Tunapaswa kujielekeza kwenye kushughulikia vyanzo badala ya matokeo. Mosi, mfumo wetu wa uchumi, uzalishaji umepungua uchuuzi umeongezeka. Ukuaji wa uchumi ni kwenye sekta zisizoajiri watu wengi.
Hivyo, lazima tukigeuze kilimo kinachoajiri wengi kuwa ni fursa ya ajira, kilimo cha sasa kinafanya kazi ya kilimo ionekani ni suluba ya kujikimu tu na hivyo kuwa sehemu ya mduara wa umaskini. Kuna haja ya kuuganisha uzalishaji wa kilimo na uchakataji (processing) kwenye viwanda vidogo vidogo vyenye muunganiko na kilimo (forward and backward linkages). Hii itapunguza kasi ya vijana kukimbilia mijini na kuongeza tatizo la ukosefu wa ajira.
Pili, kwa upande wa vijana ambao wako tayari mijini lazima kuwapa fursa ya mitaji waweze kujiajiri itayotanguliwa kwanza na mafunzo ya ujasiramali na uzalishaji na sio ya uchuuzi peke ambayo inageuza vijana wengi kuwa Machinga. Tufanye vijana wengi wawe wazalishaji kwa kujiajiria na kutoa huduma.
Tatu, kwa mijini lazima kufufua viwanda vilivyouwawa na kufungua vingine vipya. Katika kufanya hivyo, sio kutazama tu viwanda vikubwa ambavyo vinatumia mitaji mikubwa lakini vijana ajiri wachache kutokana na teknolojia, tujikite katika viwanda vidogo pia kuweza kuajiri wengi.Nguvu kubwa imepelekwe kwenye sekta ya umma
Nne, kwa wale ambao wako kwenye mfumo wa elimu bado na wanaotarajia kuanza elimu, lazima kuboresha elimu yetu kuwezesha wahitimu kuweza kumudu ushindani wa kujiajiri na kuajiriwa.
Tano, kwa wahitimu wenye uwezo na kwa fursa za kazi zilizopo kwenye sekta ya umma na binafsi, kigezo cha uzoeefu kusiwe tena cha lazima bali cha motisha. Na Serikali itoe motisha maalum kwa vijana wanaojiajiri na wote wenye kutoa kipaumbele katika kuajiri vijana. Hata yote na mengine yanahitaji Mpango Maalum wa kuwezesha ajira kwa vijana utakaohusisha tathmini ya utekelezaji wa sheria ya kuongeza ajira ya 1999 (employment promotion Act) na kutenga rasilimali za kutosha.
Kama tulitenga zaidi ya trilioni kunusuru uchumi, kwa nini hatutengi trilioni kupunguza tatizo la ajira. Kiwango cha fedha kilicho mikokoni mwa mwa mafisadi kingetosha pia kufanikisha azma hii. Ni muhimu pia kwenye mikataba ya matumizi ya fedha za umma kama ya ujenzi nk, kipengele cha kuwezesha ajira kwa vijana kikawa sehemu ya mikataba hiyo ikiwemo ya kwenye rasilimali za chini kama madini na gesi.

No comments:

Post a Comment