ZITAMBUE MBINU 14 ZITAKAZOKUSAIDIA KUJIAMINI KATIKA MAISHA YAKO
Kila
kitu ambacho ni halisi kinawezekana. Bila shaka unakumbuka vizuri
kuhusu namna kutojiamini kwetu kunavyojengwa. Kwa kuwa tunajua chanzo,
ni rahisi kupata tiba.
Njia
zifuatazo zinaweza kukusaidia katika kujenga kujiamini. Kuna njia
nyingi zinazopendekezwa, lakini kuna zile ambazo zimetumika sana katika
kufanya kazi hiyo. Hizi zifuatazo ni baadhi yake.
1. Yachunguze
mawazo yako na vitendo vyako kwa uangalifu ili kujua ni kitu gani
hukufanya usisimke. Anza kufanya mambo ambayo unaona kwamba una uwezo
kuyafanya bila wasiwasi na kuchukua uamuzi unaojitegemea kufuatana na
utashi wako. Ikibidi unaweza kuomba msaada wa wengine, lakini jaribu
kila mara kufanya mambo kufuatana na unavyoyaona.
2. Jifunze
kujithamini. inawezekana kwa miaka na miaka umekuwa unajiona kama mtu
usiye na thamani. Pia unaweza ukaona kwamba, hadhi uliyokuwa nayo mbele
ya
ndugu, jumuiya na jamii imepungua. Jali ujuzi na vipaji vyako; hata
kama kuna ndugu wametajirika pamoja na kuwa ni mbumbumbu hiyo isiwe
chanzo cha kukuvunja nguvu. Iko siku utafanikiwa kama utaanza kujiamini.
3. Jisamehe bila masharti yoyote. Kama maisha yako ya awali yalikuwa si ya kiungwana, jisamehe na anza maisha yako upya. Njia bora ya kujisamehe ni kujipenda bila masharti yoyote.
4. Pambana
na hofu. Hofu ni kitu kibaya sana kwa sababu inaingilia kwenye uwezo
wako wa kufikiri. Ili ufanikishe malengo yako ya maisha huna budi
kuhakikisha kuwa huna hofu tena.
5. Fanya
vitu unavyoviogopa. Orodhesha idadi ya vitu ambavyo ulikuwa
unaviogopa. Kisha anza na vitu ambavyo unaviogopa zaidi na jiulize kwa
nini usiweze kuvifanya.
6. Jifunze
kupambana na kushindwa. Kubali kwamba kushindwa ni kama chombo cha
kujifunzia na si kitu cha kukukatisha tamaa. Jua, na amini kwamba, bila
kushindwa hakuna kukua. Pia elewa kwamba, kushindwa siyo dalili ya
udhaifu, bali uimara.
7. Kubali
kupingwa kwa moyo mkunjufu. Watu wa nje wanaweza kukusaidia kwa mambo
yako mengi ambayo huyaoni. Watu wakikusoa, hata kama ni kifedhuli,
chukua yaliyo mema na yafanyie kazi.
8. Fanya
mazoezi ya kujiamini. Jifunze kusimama kwa miguu yako mwenyewe
kimawazo, kiimani na kimatendo. Bila kuonyesha ujeuri unaweza kulinda
haki zako, matarajio yako na maadili yako. Anza kujifunza kujenga
taswira ya kujiona uko mwenyewe na unamudu kila kitu. Bila msaada na
utegemezi kwa wengine.
9. Jipongeze
kwa maneno mazuri. Jiamini na daima jipe moyo kwa maneno ambayo
yatakutia moyo ili kwenda vyema katika shughuli zako. Usitumia maneno ya
kejeli, kashfa na chuki dhidi yako mwenyewe, ‘mimi ni mjinga kweli
yaani jambo
dogo kama hili limenishinda….’ Unaweza kujisemea baada ya kukosea.
Kama umekosea, jiambie maneno mazuri ya kujipa moyo na siyo maneno ya
kero na fadhaa.
10. Usijilinganishe na wengine, bali
iga. Kama wengine wanakuzidi isikukatishe tamaa ila iwe ni chachu ya
maendeleo . jiambie, ‘kama wanaweza, maana yake ni kwamba, inawezekana,
nami nitaweza tu.’
11. Fikiria
mambo ambayo yanakufanya usiwe na furaha na jaribu kupambana nayo na
kuondokana nayo. Kila wakati jiulize, ni kwa nini uko kwenye hali ya
kihisia uliyo nayo. Usikubali kufuga huzuni kwa muda mrefu ndani mwako.
12. Fanya
mambo uyapendayo zaidi. Kujiamini kutaongezeka kama utafanya mambo
unayoyafahamu zaidi kwa sababu ni rahisi kuyafanikisha na kukuletea
furaha.
13. Jifunze
namna ya kushughulikia hasira zako. Mtu asiyejiamini ana kawaida ya
kutaka kupendwa na watu, na katika kufanya hivyo, hapendi kuonekana kuwa
ni mtu mwenye hasira na hivyo kuendelea kubakia na hasira zake moyoni
hata kama ameudhiwa.
14. Kuzuia
hasira hakusaidii, zaidi ya kukuongezea kuchanganyikiwa na kukufanya
kuwa mtu usiye na furaha au kisirani. Ukiudhiwa, mwambie aliyekuudhi
kinaganaga, lakini katika mazingira ya kistaarabu ambayo hayawezi
kukuumiza wewe wala mtu ambaye amekuudhi.
No comments:
Post a Comment