Dodoma. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama chake hakitavumilia vitendo vya usaliti na kwamba mwanachama yeyote atakayekiuka maagizo ya chama hicho atachukuliwa hatua kali.
“Katika hili hatutakuwa na mchezo na naomba niweke wazi kabisa kwamba usaliti hausameheki. Tuna vikao vya chama vinakuja siku za karibuni mtu yeyote ambaye atabainika kusaliti uamuzi wa chama, uwe wa Kamati Kuu au mwingine wowote, tutachukua hatua hata kama ni kumfukuza uanachama,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo alikuwa akizungumzia taarifa za kuwapo bungeni, Dodoma kwa baadhi ya wanachama wa Chadema, kinyume cha makubaliano ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wabunge hao ni Leticia Nyerere (Viti Maalumu), John Shibuda (Maswa Mashariki) na Said Arfi (Mpanda Mjini) ambaye aliwasili jana na kwenda kushiriki kwenye kikao cha kamati namba 10 kilichokuwa kikifanyika Ukumbi wa Internet, Chuo cha St. Gaspar.
Mbowe alisema baada ya viongozi wakuu wa Ukawa kukubaliana kwamba hawatashiriki katika awamu ya pili ya Bunge Maalumu, kila chama kiliwaelekeza wabunge wake kuhusu msimamo huo ambao pia uliridhiwa na vikao vya vyama husika.
“Sisi suala hili limepitishwa na Kamati Kuu ya Chadema, sasa wewe ni nani kukataa, kupinga au kwenda kinyume cha matakwa ya Kamati Kuu? Ole wake mtu atakayethubutu kushiriki hivyo vikao vya Kamati za Bunge,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Wakati tunagombea ubunge 2010 hakukuwa na ahadi kwamba kutakuwa na Bunge la Katiba, hili limetokea tu, sasa kama sisi kwa masilahi mapana ya umma tunauona mchakato hauko sawa, kwa nini wewe ulazimishe kushiriki, unakwenda Dodoma kumwakilisha nani?”
Vyama vingine vyenye wabunge ambavyo pia wanachama wake wamesusia Bunge Maalumu ni NCCR Mageuzi na CUF. Kadhalika Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila ni miongoni mwa waliosusia vikao hivyo.
No comments:
Post a Comment