Saturday 2 August 2014

TULIKUWA SAHIHI KUSUSIA BUNGE LA KATIBA

Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (pichani) amewataka viongozi kuacha kufananisha mchakato wa Katiba na ushabiki wa mpira wa Simba na Yanga.
Zitto alitoa kauli hiyo jana wakati wa majadiliano kwenye Kipindi cha Tuongee Asubuhi kinachorushwa na kituo cha Star Tv.
Alisema, majadiliano ya mchakato wa katiba yasifananishwe na mabishano ya mpira wa Yanga na Simba, kwani mchakato huo ni nyeti na unahitaji maridhiano ya kitaifa.
“Mashindano ya kisiasa hayafai wakati huu...viongozi wanatakiwa kukaa chini kuzungumza na kuridhiana katika mambo ya msingi.Hata kama kuna baadhi watapishana ni sawa, lakini wahakikishe wanakubaliana kwa asilimia 90. Suala la katiba ni jambo la msingi kwa mustakabali wa taifa hili,” alisema Zitto.
Alisema kilichosababisha wabunge zaidi ya 200 ambao ni Ukawa, kususia vikao vya Bunge hilo Aprili  ni kitendo cha Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta  na Makamu  wake, Samia Suluhu Hassan kushindwa kuhakikisha kwamba kanuni zinafuatwa wakati wa vikao.
 “Mwenyekiti na msaidizi wake walipitiwa…walishindwa kukemea lugha za kejeli na matusi zilizokuwa zinatolewa na baadhi ya wajumbe ndani ya vikao vya Bunge hilo licha ya kuwapo kwa kanuni ambazo zinakataza matumizi ya lugha hizo ndani Bunge,” alisema Zitto na kuongeza:
“Viongozi wa dini na wazee pia hawakukemea wakati kauli hizo zinatolewa na baadhi ya wajumbe.”
Wakati vikao vya Bunge hivyo vilipokuwa vinaendelea baadhi ya wajumbe kutoka CCM na wajumbe 210 walioteuliwa na Rais walitumia lugha za matusi na kejeli kuwabeza wajumbe wa Ukawa waliokuwa wanatetea mfumo wa serikali tatu ambao umependekezwa katika Rasimu ya Jaji Joseph Warioba.
Lakini Zitto, ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba alisema huu siyo wakati wa kutupiana lawama tena, “Ukawa hawakufanya kosa…hivi sasa hatuna budi kukubali kwamba makosa ya kutofuata kanuni yameshatendeka, lakini tumejifunza. Tukirejea tena ni lazima kanuni zizingatiwe. Pia tujadili masuala ambayo yapo ndani ya Rasimu ya Katiba ili tupate Katiba Bora.”

No comments:

Post a Comment