MWENYEKITI
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe,
amewekewa pingamizi la kutogombea nafasi hiyo kwa awamu ya tatu kwa
madai ya kukiuka katiba ya chama hicho na maagizo ya Msajili wa Vyama
vya Siasa nchini.
Pingamizi hilo limewekwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora, Kansa Mbarouk, ambaye pia ni mgombea wa nafasi hiyo.
Barua
ya Mbarouk yenye kumbukumbu namba Mbarouk/UCH/14 kwenda kwa Katibu
Mkuu wa Chadema na Msajili wa Vyama vya Siasa, iliyoandikwa Septemba
tano, inasema kufikia Septemba 14 siku ya uchaguzi mkuu wa chama hicho,
Mbowe atakuwa ametumikia vipindi viwili katika nafasi ya mwenyekiti wa
taifa.
Barua
ya Mbarouk inasema kwa mujibu wa katiba ya Chadema, kama
ilivyothibitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, hakuna mwanachama
anayeruhusiwa kuchaguliwa kuongoza kwa zaidi ya vipindi viwili katika
cheo kimoja kwa ngazi moja.
“Msajili
wa Vyama alikuwa ametoa maelekezo kwamba chama kiitishe Baraza Kuu na
Mkutano Mkuu Maalumu kwa lengo la kubadilisha kipengele kinachoweka
ukomo wa uongozi kama litaona kuna haja hiyo kabla ya kufanyika uchaguzi
mkuu. Hata hivyo hadi naandika barua hii hakuna dalili zozote kwamba
mkutano mkuu maalumu utaitishwa na maandalizi ya uchaguzi yanaendelea
bila kujali agizo la msajili wa vyama,”alisema Mbarouk katika barua hiyo.
Alisema katika kipindi chake cha uongozi Mbowe alisimamia vikao vya chama vilivyofanya maamuzi ya kuvunja katiba waziwazi.
“Mfano
Novemba 2013, Mbowe alisimamia kikao cha kamati kuu kilichomvua nafasi
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama, Zitto Kabwe na wenzake bila
kuzingatia mamlaka ya kikao hicho. Kwa mujibu wa Sura ya Sita ibara ya
6.3.6(b) ya katiba ya Chadema toleo la mwaka 2006 ‘kiongozi aliyeteuliwa
na vikao vya uongozi ataweza kusimamishwa au kuachishwa uongozi na
kikao kilichomteua’,”alisema.
Alisema
baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 chama kilipata nafasi tano za kuteua
nafasi wabunge wa viti maalumu kuingia katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano, ambapo Kamati Kuu kilipitisha majina ya Suzan Kiwanga, Chiku
Abwao, Halima Mdee, Mhonga Ruhanywa na Grace Kiwelu lakini Mbowe
alibadilisha majina hayo.
“Mbowe
alibadilisha majina ya Chiku Abwao na Susan Kiwanga huku akiwapachika
Susan Lyimo na Lucy Uwenya. Baadaye Mbowe alikiri kosa na kuomba msamaha
katika kikao cha Kamati Kuu,”alisema.
Alisema
hayo yote yanadhihirisha pasipo shaka kwamba mwenyekiti huyo amekosa
uaminifu hivyo anapaswa kunyang’anywa nafasi hiyo ya uenyekiti.
“Ninatambua
kuwa kwa mujibu wa katiba ya chama Sura ya Saba ibara ya 7.3.1,
uchaguzi ngazi ya taifa unapaswa kusimamiwa na wazee wastaafu wa chama
hata hivyo hadi naandika barua hii sina taarifa kuhusu kuteuliwa kwa
kamati hii. Hivyo basi nimelazimika kuandika barua yangu ya pingamizi
kwako nikiamini kwamba utaifikisha katika chombo husika
kinachoshughulikia uchaguzi,”alisema Mbarouka.
Alipotafutwa
kupitia simu yake ya kiganjani kuzungumzia barua hiyo, Mbarouk alisema
ni kweli ameandika barua hiyo na kwamba aliikabidhi juzi Septemba 6
katika ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama.
“Ni kweli nimeiandika mimi na nilikabidhi jana (juzi) katika ofisi ya katibu mkuu wa chama,”alisema Mbarouk.
Kwa
upande wake Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alipoulizwa endapo
ni kweli barua hiyo imewafikia, alimwambia mwandishi wa habari hizi
kuwa atampigia baadaye.
Hata
hivyo baada ya Makene kumpigia simu mwandishi alimtaka amtajie lengo la
Mbarouk kumpinga Mbowe, baada ya mwandishi kufanya hivyo aliahidi
angepiga tena simu, lakini hadi Habari hii inakwenda hewani hakupiga
simu.
No comments:
Post a Comment