Monday 12 August 2013

SHEIKH PONDA YUKO CHINI YA ULINZI MKALI HOPITALINI DAR


Jumuiya ya Taasisi za kidini za Kiislamu nchini Tanzania imeitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini na kuwachukulia hatua watu waliompiga risasi Sheikh Ponda Issa Ponda Jumamosi mjini Morogoro, Mashariki mwa nchi hiyo.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Alhajj Mussa Kundecha, amewaambia waandishi wa habari jijini Dar kuwa endapo serikali haitachukua hatua itakayowaridhisha Waislamu, wataamua kufikiria upya mustakabali wao na serikali ya Tanzania.
Sheikh Ponda amelazwa katika hospitali ya taifa, Muhimbili, mjini Dar es Salaam akiuguza jeraha la risasi huku akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu.

Msemaji wa Jeshi la polisi nchini humo Advera Senso alisema kuwa jeshi lake kwa kushirikiana na jukwaa la haki jinai wameunda kikosi kazi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa tukio hilo huku akikana kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi na polisi.
Senso amewalaumu wafuasi wa Sheikh Ponda kwa kuwazuia askari kumkamata Sheikh huyo kwa kuwarushia mawe; hatua iliyosababisha askari hao kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya na hata hivyo wafuasi hao walifanikiwa kumtorosha kiongozi huyo wa kidini.

Taarifa za jumuiya hiyo ambayo inajulikana zaidi Tanzania kama Shura ya Maimamu zinasema kuwa Sheikh Ponda ambaye polisi wanasema walikuwa wakimtafuta kwa tuhuma za kutoa matamko ya uchochezi, alisafirishwa usiku kutoka mji wa Morogoro hadi Dar es Salaam zaidi ya kilomita 200.
 

No comments:

Post a Comment