Friday, 6 September 2013

Dimpoz amtaja TID kuwa mwalimu wake


Asema ndio siri ya yeye kufanikiwa katika shughuli zake za muziki. Aamekuwa mfano wa kuigwa kwa namna anavyoendesha muziki kistaarabu na katika hali yenye ufanisi mkubwa.
Dar. Msanii anayetamba na wimbo wa Nai Nai, Me and You, Faraji Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz ameanika hadharani siri za mafanikio yake katika semina ya Fursa iliyofanyika mkoani Mtwara wikiendi iliyopita, ambapo alisema alijifunza muziki miaka 10, kabla ya kuingia rasmi katika muziki.
“Nilikuwa na ndoto za kuja kuwa mwanamuziki mkubwa sana, lakini sikuwa na uwezo wa kuyafikia mafanikio hayo kwani sikuwa na ujuzi wowote, lakini hivi sasa nashkuru Mungu kwani niliitumia fursa ambayo leo hii imenipa mafanikio niliyokuwa nayaota.”
Ommy Dimpoz anayesisitiza wasanii wasikurupuke kuingia kwenye muziki kabla ya ujuzi, amefafanua zaidi namna alivyoanza kuonekana “Nilitumia miaka yangu mitano nikiwa chini ya mwanamuziki Khalid Mohamed ‘TID’ huko nilijifunza yaliyo mengi ambayo yamenijengea msingi imara.
“Unajua unapokuwa unajifunza unakuwa kama upo gereji maana unalifungua gari na kulifunga upya, nilipopata fursa ile niliitumia vilivyo sikuhitaji kunung’unika kwani nilijua nini nafanya na nahitaji nini, japokuwa ni miaka mingi ila nilitoka pale nimeiva ndio maana leo hii nasimama kama msanii ninayejitegemea,” anasema.
Amesema wasanii wengi wanaingia katika muziki kwa kukurupuka ndio maana wanashindwa kuhimili katika soko la muziki.
“Mfano mwingine ni Diamond, sisi ni wasanii tuliojifunza kwa muda mrefu muziki ndio maana mpaka leo tupo vizuri, nashukuru nilijifunza na wadau wa muziki nao wakaniona kupitia bendi hiyo,” anasema.
Amefafanua kuwa wakati amefanya maamuzi ya kujiengua katika bendi ile, alitoa wimbo wake mpya Nai Nai ambao anakiri kuusambaza pasipo kutumia fedha yoyote.
“Nilisambaza Nai Nai bila kulipa gharama yoyote, kila mtu aliyeusikia wimbo ule aliupenda, nilipigiwa simu na vyombo mbalimbali vya habari wakihitaji nipeleke kazi zangu, haikuwa rahisi kwangu kwa kuwa nilipata ujuzi kabla ya kuingia kwenye muziki.”

No comments:

Post a Comment