Saturday 28 September 2013

Kiama cha wauza unga chaja, faini kuondolewa, kifungo ni cha maisha

Dar es Salaam. Serikali imependekeza marekebisho ya sheria ya kudhibiti dawa za kulevya itakayotoa hukumu ya kifungo cha maisha na kufuta kipengele kwenye sheria ya sasa kinachompa mshtakiwa nafasi ya kulipa faini.
Sheria iliyopo sasa ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya ya mwaka 1995 (Sura ya 95, Ibara ya 16) inasema, endapo mtu atakamatwa kwa kosa la kumiliki, kusafirisha, kuzalisha au kutengeneza mashine ya dawa za kulevya, atahukumiwa kifungo cha maisha jela au kulipa faini ya Sh10 milioni.
Hatua hiyo inakuja wakati idadi ya Watanzania wanaosafirisha, kuzalisha na kutumia dawa hizo ikiongezeka hapa nchini.
Pamoja na mapendekezo hayo, wadau mbalimbali wamesema kufanyika kwa maboresho hayo hakutasaidia kupambana na tatizo lililopo hivi sasa, ikiwa maadili ya wananchi na viongozi yaliyoporomoka hayatarekebishwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Kitila Mkumbo alisema sheria yoyote itakayowekwa haiwezi kuwa ‘mwarobaini’ wa kutibu tatizo la dawa za kulevya hapa nchini kama wanaohusika hawatawajibishwa.
“Hivi sasa zipo sheria, lakini hazitekelezwi. Kuna baadhi ya viongozi wakubwa kabisa wametajwa kujihusisha na dawa za kulevya, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa,” alisema Mkumbo.
Mbunge wa Kawe na Mjumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge, Halima Mdee, alisema Tanzania ina sheria nzuri na bora, lakini changamoto ipo katika utekelezaji wake kwa kuwa rushwa ina mchango mkubwa katika kudhoofisha maendeleo ya taifa.
Mdee alisema ingawa sheria ya rushwa iliyopo hivi sasa ni nzuri, ina kasoro kadhaa zinazohitaji kufanyiwa marekebisho ili kuipa nguvu zaidi.
Alisema baadhi ya viongozi waliopewa dhamana na wananchi wanatuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
“Kama mtandao wa dawa za kulevya tunaousikia upo kuanzia viongozi wakubwa hadi wa chini, unadhani hata ukiwa na sheria nzuri itatekelezwa na nani? alihoji Mdee.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alisema mapendekezo ya sheria ya dawa za kulevya ni mazuri, lakini yana changamoto nyingi katika utekelezaji wake.
Alisema ingawa sheria mpya inayopendekezwa inataja adhabu ya juu kuwa ni kifungo cha maisha kwa mtu anayejihusisha na biashara ya dawa za kulevya, haijaweka wazi kiwango cha chini kwa mtuhumiwa atakayepatikana na kosa hilo.
“Kwa namna ilivyo sasa, sheria hii inaweza kuleta shida kwa sababu haitaji ‘minimum sentence’ (kiwango cha chini cha hukumu), hivyo mtu anaweza kusema mtuhumiwa afungwe mwaka mmoja,” alisema Nzowa.
Nzowa alisema sheria ya dawa za kulevya iliyopo inaweka kiwango cha chini cha adhabu kuwa kisiwe kifungo cha chini ya miaka ishirini.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema kinachotakiwa si sheria kali, bali viongozi wawajibike kwa kuwa kuna baadhi ya watu walikamatwa na vidhibiti lakini wameachiwa huru.
“Sheria kali zitakuwa kwa ajili ya wafanyabishara wadogo tu kwa sababu wale wakubwa wana fedha nyingi, ndiyo maana tunahitaji viongozi kama Dk Harrison Mwakyembe (Waziri wa Uchukuzi)wanaopambana, ingawa anaonekana kama anapigana na maji yanayomrudisha nyuma,” alisema Dk Kijo-Bisimba.
Mmoja wa vijana walioathiriwa na dawa za kulevya, ambaye hakupenda kutaja jina lake kwa sababu za usalama, alisema sheria kali hazitasaidia chochote, kwa sababu wafanyabiashara wakubwa ndiyo wanaotoa rushwa ili waendelee kufanya biashara hiyo.
“Kama kweli wanataka biashara ya dawa za kulevya iishe kabisa hapa nchini, waanze kwanza kutokomeza rushwa,” alisema.
Mwanamke mmoja ambaye ametumia dawa za kulevya kwa muda mrefu, ambaye pia aliomba jina lake lisitajwe gazetini, alisema sheria hiyo ni kali na kwamba kama itatekelezwa kikamilifu ‘mateja’ wengi ndiyo watakaopelekwa gerezani, kwa sababu wengi wao ni maskini.
“Ninachoona sheria hii itaongeza viwango vya kutoa rushwa kwa viongozi wasio waaminifu na kuwaacha watumiaji wengi maskini wakiozea jela,” alisema.
Jitihada zaidi
Mbali na mapendekezo ya kuboreshwa kwa sheria ya dawa za kulevya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisema Serikali pia imetoa mapendekezo ya kuundwa kwa chombo maalumu kitakachokuwa na mamlaka kamili ya kumshtaki mtuhumiwa.
“Tume ya Kuratibu Dawa za Kulevya haina mamlaka kisheria ya kukamata, kukagua na kumfikisha mtu mahakamani na badala yake majukumu hayo yako kwa Kikosi Maalumu cha Jeshi la Polisi(Task force),” alisema.
Aidha, Lukuvi alisema mbali na kuwapo kwa kikosi hicho kinachoshirikiana na tume kutekeleza majukumu hayo, changamoto bado ni kubwa.

No comments:

Post a Comment