Sunday 24 August 2014

JK: TECKNOLOGIA YA MAWASILIANO KUTUMIKA KTK HUDUMA ZA AFYA

Rais Jakaya Kikwete, ameahidi kuboresha sekta ya huduma ya afya vijijini katika zahanati na vituo vya afya kwa kuweka huduma ya matibabu ya mtandao.
Huduma hiyo itafanya mawasiliano moja kwa moja na madaktari bingwa kutoka ndani na nje ya nchi wakati wa kutoa matibabu yakiwamo ya upasuaji.

Alisema hayo wakati wa ziara yake mkoani Morogoro na kuzungumza na wananchi wa vijiji vya Kisaki, Dutumi, Matombo na Kinole vilivyopo katika halmashauri ya wilaya ya Morogoro vijijini.

Alisema huduma hiyo itasaidia kupunguza vifo vya wagonjwa hasa akina mama wajawazito na watoto.

“Hivi sasa tunataka kumaliza matatizo ya vifo vingi ambavyo vinatokea katika zahanati na vituo vya afya kutokana na kukosekana kwa watalaam wa kutosha, kwa kutumia huduma ya matibabu kwa njia ya mtandao mganga aliopo katika kituo cha afya atakuwa akiwasiliana kwa ushauri na daktari bingwa kutoka Muhimbili, Bugando na sehemu nyingine anapotokea mgonjwa mwenye tatizo kubwa,” alisema.
Alisema huduma ya mtandao imeonyesha mafanikio yakiwamo ya madaktari waliopo ngazi ya chini kuwasiliana kwa njia ya simu na madaktari bingwa inapotokea dharura na hivyo mgonjwa kupatiwa matibabu ya haraka.

Rais Kikwete alisema kuwa kutokana na hali ya zahanati na vituo vingi vya afya kukosa madaktari bingwa, huduma hiyo itakuwa mkombozi mkubwa katika kuokoa maisha ya wagonjwa maeneo ya vijijini.

Alisema huduma hiyo imeshaonyesha mafanikio makubwa katika hospitali ya tarafa ya Mwaya wilaya ya Ulanga ambako imeanza kwa majaribio na kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na watoto.

Alisema kati ya kinamama 259 waliofanyiwa upasuaji kupitia huduma hiyo wawili tu ndiyo walipoteza maisha.

Alisema kuwa ili kufikia malengo hayo kwa nchi nzima serikali itaongeza bajeti ya afya na kutafuta wafadhili na wahisani mbalimbali kwajili ya kusaidia mfumo hasa katika maeneo ya vijijini ili kupunguza vifo hivyo.

Hata hivyo, Rais Kikwete aliwaagiza madaktari wa wilaya hapa nchini kuhakikisha wanaweka mipango na mbinu mbadala ikiwamo za kujenga wodi kwa ajili ya kusubiria kinamama wajawazito ambao wengi wao wanatoka katika maeneo ya vijijini ikiwa ni njia ya kupunguza vifo hivyo.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment