Vyumba
20 vya bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari ya African Muslim,
iliyoko Kata ya Kaloleni, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro,
vimeteketea kwa moto.
Moto
huo ambao ulizuka juzi saa 1:45 jioni na kuwaka kwa zaidi ya saa tano,
ulianzia katika choo cha shule hiyo, jirani na Bweni la Makka kabla ya
kuruka kwenye chumba cha jirani na kusambaa kwenye vyumba 20 vilivyoko
katika bweni hilo.
Akizungumza
toka eneo la tukio, Mkurugenzi wa Shule hiyo, Ali Adam Ali, alisema
moto huo ambao hadi sasa chanzo chake hakijajulikana japo inadaiwa kuwa
ni hitilafu ya umeme, umesababisha hasara kubwa kwa wanafunzi zaidi ya
96 wa kidato cha nne wanaotumia bweni hilo.
“Moto
huu ulianza majira ya saa mbili kasoro, wanafunzi walikuwa wanajiandaa
kuingia katika swala ya Isha, mmoja wa wanafunzi alihisi harufu ya moto
na kuwajuza wenzie, baadae wakaanza kuhangaika kutafuta ni wapi chanzo
chake kilipo, waligundua kuwa ulianzia chooni, ghafla ukasambaa katika
vyumba vingine vya ghorofani kupitia chumba cha jirani na choo,” alisema Ali.
Alisema
hakukuwa na madhara makubwa yaliyotokana na moto huo kutokana na
wanafunzi wengi kuwa likizo, na kwamba ni wanafunzi wa kidato cha nne na
kidato cha pili tu ndio walioathirika na moto huo.
“Hakuna
majeraha makubwa kutokana na tahadhari ya kiusalama tuliyochukua kwa
kushirikiana na uongozi wa Serikali ya Mtaa, wanafunzi walijitahidi
kuondoa vitu vyao, vitanda na mabegi ya baadhi yao vimeungua katika
moto, wanafunzi wanne walipoteza fahamu, tuliwakimbiza hospitali na sasa
wanaendelea vizuri,” alisema Ali.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Dkt. Ibrahim Msengi, aliuagiza uongozi wa shule hiyo
kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa na Ofisa Elimu wa mkoa
kufanya tathimini ya hasara iliyotokana na moto huo.
Wakati
huo huo, Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Kilimanjaro, Estomih Makyara
amemtaka mkurugenzi wa shule hiyo kutoa wiki moja ya mapumziko kwa
wanafunzi walioathirika na moto huo, isipokuwa wanafunzi wa darasa la
saba wanaoendelea na mitihani wataendelea kama kawaida
No comments:
Post a Comment