Monday 30 September 2013

TAARIFA KUTOKA MAKAO MAKUU YA JESHI LA MAGEREZA KUJA KWA WATANZANIA WOTE

Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuzingatia Kifungu cha 3(2) Act NO. 8/1990 cha Sheria ya Polisi na Magereza ya Mwaka 1990 amewapandisha vyeo Maafisa wa Jeshi la Magereza 22 waliokuwa katika ngazi ya Kamishna Msaidizi wa Magereza kuwa Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Magereza.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa leo Septemba 30, 2013 na Ofisi ya Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, Makao Makuu ya Magereza, Dar es Salaam inasema kuwa kupandishwa kwao vyeo hivyo kunaanzia tarehe 13 Septemba, 2013.
  Aidha, taarifa hiyo imeongeza kuwa taratibu za uvalishaji wa vyeo hivyo zitafanyika katika Chuo cha Maafisa Magereza Ukonga tarehe 5 Oktoba, 2013 saa 10:00 jioni.
 Kufuatia kupandishwa vyeo kwa Maafisa hao Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini(CGP) John Casmir Minja amewapongeza wale wote waliopandishwa vyeo na kuwataka kuendelea kutenda kazi zao kwa ubunifu, kasi zaidi na ufanisi ili waendelee kuongezewa Madaraka zaidi. Aidha Madaraka hayo waliyopewa ni miongoni mwa mikakati inayoendelea hivi sasa katika Maboresho ya kulijenga Jeshi la Magereza kuwa la Kisasa ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa Weledi zaidi.
Imetolewa na Inspekta Lucas Mboje,
Afisa Habari wa Jeshi la Magereza,
Makao Makuu ya Jeshi la Magereza,
Tarehe 30 Septemba, 2013.

No comments:

Post a Comment