Sunday, 3 August 2014

Umoja wa Katiba ya Wananchi wasisitiza kutorudi Bunge

KAMA ndivyo, huenda Bunge Maalumu la Katiba, linalotarajiwa kuanza awamu ya pili ya vikao vyake keshokutwa mjini Dodoma, litafanyika bila ya kuwa na wajumbe kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
 
Hali hiyo inatokana na kauli ya Ukawa, inayoundwa na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani na wafuasi wao, kwamba hawatashiriki katika Bunge hilo na kwenda mbali zaidi, wakidai hawana mpango wa kuwa na vikao vya maridhiano dhidi ya wenzao wa chama tawala, CCM baada ya kikao kingine cha juzi, kilichokuwa cha nne, kukwama.
 
Kauli ya Ukawa ilitolewa jana, mbele ya waandishi wa habari na viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda umoja huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
 
Kwa pamoja, walisema wameridhia kujiweka kando katika Bunge na vikao vya maridhiano. Chama cha NLD kinachoongozwa na Dk Emmanuel Makaidi, nacho kimejiweka kando.
 
Mbowe alifafanua kuwa baada ya kikao cha nne cha maridhiano kati ya umoja huo na CCM, kilichofanyika juzi chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuvunjika, wametafakari kwa kina na kubaini kurejea bungeni kuendeleza mivutano, hakutakuwa na tija kwa Taifa.
 
“Hivyo tumeazimia kutorejea tena katika Bunge la Katiba wala kushiriki mazungumzo yoyote kuhusu suala hilo, kutokana na ukweli kuwa mazungumzo haya yaliyovunjika, yalikuwa ya kuwezesha kupata Katiba bora, lakini CCM waliyafanya kuwa yenye maslahi ya chama chao, siyo Taifa.
 
”Na baada ya awamu nne za vikao vya mazungumzo kati yetu na CCM, Ukawa tunatangaza kwamba hatuko tayari kuendelea na mazungumzo na CCM wala kurudi katika mkutano wa Bunge Maalumu la Katiba, kwa kuwa kufanya hivyo ni kusaliti maoni ya wananchi na kutumia vibaya fedha za umma,” alisema Mbowe.
 
Kauli ya CCM Hata hivyo, kwa mara nyingine jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema chama chake hakijashangazwa na uamuzi huo, kwa kuwa walifahamu Ukawa hawana hoja za msingi, hivyo wamekimbia aibu.
UKAWA
 
“Hata kwenye vikao, hawakuwa na kitu kipya, ni malalamiko tu huku wakishindwa kujenga hoja, kwa hiyo tulijua hawa wenzetu lazima mwisho wa siku wakimbie aibu yao…ni aibu tu imewashika, ndiyo maana wamepatafuta pa kutokea,” alisema Nnauye.
 
TUCTA na Katiba mpya Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi nchini (TUCTA), Nicholaus Mgaya amezungumzia Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Semina ya Wanawake wa shirikisho hilo.
 
Mgaya alisema anasikitishwa na mwenendo wa Bunge hilo, ikiwemo kwa wajumbe wake kushindwa kufikia muafaka.
 
“Sisi tuna wawakilishi wetu 19 kutoka Tanzania Bara na Visiwani, ila tunasikitika baadhi ya wajumbe wameacha kujadili mambo tuliyowatuma, tungependa wajumbe wa Bunge hilo wajikite kwenye kujadili rasimu iliyopo, waachane na matusi na kejeli,” alisema

No comments:

Post a Comment