Tuesday 26 August 2014

wenye dalala na UDA wamesaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano

UONGOZI wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) na wamiliki wa daladala mkoani humo, wamesaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano ili kushinda zabuni ya kuendesha Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (DART).

Utiaji saini huo ulifanyika Dar es Salaam juzi kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere ukishuhudiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bi. Hawa Ghasia pamoja na na Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Said Meck Sadiki.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bi. Ghasia alisema uamuzi uliochukuliwa na UDA pamoja na wamiliki wa daladala ni mfano wa kuigwa nchini.

Alisema kuungana kwao pamoja, kutawajengea mazingira bora ya kuaminika zaidi na kutoa ushindani madhubuti dhidi ya kampuni za nje ambazo zitajitokeza kuomba kuendesha mradi wa DART.

Alimpongeza Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Saimon Group, Bw. Robert Kisena na viongozi wa vyama vya wamiliki wa daladala mkoani humo kwa uamuzi huo wenye tija kwa Taifa kwani utaongeza ajira na kupunguza umaskini.

Uamuzi huo ulifikiwa baada ya mkutano uliokuwa na mafanikio makubwa uliofanyika jijini humo hivi karibuni katika Ukumbi wa Karimjee ulioandaliwa na Kamati Teule ya Wamiliki wa Daladala.

Kwa upande wake, Bw. Sadiki alisema kuunganisha nguvu kwa wadau hao kutatoa fursa kwa Serikali kuwaunga mkono katika jitihada zake za kuboresha hali ya usafiri katika jiji hilo.

"Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na wazawa kwani haiwezi kutumia mabilioni ya fedha kujenga barabara hizo halafu mtu wa kuziendesha atoke nje, hii itakuwa aibu na dharau.

"Kuungana kwenu, kutaishawishi Serikali baada ya kutangazwa zabuni, ianze kuwafikiria nyinyi kwa kuwapa kipaumbele kwani hii ni ishara kwamba, mmedhamiria kupambana katika zabuni," alisema Bw.Sadiki.

Naye Bw. Kisena, alisema watafungua milango kwa wamiliki hao kununua hisa ambazo zitamwezesha mtu yeyote kuwa Mkurugenzi.

"Tunatoa wito kwa wananchi mbalimbali, wajitokeze kununua hisa kwa wingi zaidi ili kuhakikisha tunaboresha huduma ya usafiri katika jiji hili," alisema Bw. Kisena.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala mkoani humo (DARCOBOA), Sabri Mabrouk, alisema UDA ni kampuni yenye uwezo hivyo kuna haja ya kuunganisha nguvu ili kuhakikisha zabuni inapotangazwa hakuna kampuni kutoka nje itakayoshinda.

"Hakuna sababu ya kumwachia mtu kutoka nje aje kuendesha mradi huu, tukikusanya mitaji tukaungana na UDA, tutaweza kuendesha mradi huu kwani hauhitaji fedha nyingi sana, tukiamua tunaweza," alisema.

 Chanzo:Majira

No comments:

Post a Comment