Thursday, 11 September 2014

ZIFAHAMU SABABU 7 ZINAZOKUFANYA UENDELEE KUKOSA PESA KWENYE MAISHA YAKO KILA SIKU

1. UNA MATUMIZI MABAYA YA PESA

Wapo watu ambao wanapopata pesa zinakuwa hazitulii kabisa mikononi mwao, kila kitu kinachopita mbele ya macho yao kinakuwa halali yao. 
Kama una tabia hii ya kufanya matumizi mabaya ya pesa elewa kabisa utaendelea kuishi maisha magumu na yale yale siku zote.


Jitahidi sana kudhibiti pesa zako na sio kudhibitiwa na pesa. 
Kumbuka unapotafuta pesa kuna muda ambapo unakuwa unatumia juhudi nyingi sana mpaka kuzipata, kwanini sasa linapokuja suala la matumizi uzipoteze kiurahisi tu, weka ulinzi kwenye pesa la sivyo utaendelea kukosa pesa katika maisha yako kila mara
2. HUNA TABIA YA KUJIWEKEA AKIBA YA KUTOSHA

Hiki ni kitu muhimu ambacho kinakufanya uendelee kukosa pesa. Kwa muda mrefu umekuwa ukiishi maisha ambayo hujiwekei akiba ya kutosha ambayo itakusaidia leo na baadae katika maisha yako.


Kama una tabia hii ya kutojiwekea akiba utakwama na utashindwa hata kuendesha miradi yako mwenyewe itakayokusaidia kuachana pengine na kuajiriwa.
 Jijengee tabia hii bora ya kujiwekea akiba zako mwenyewe na kama huwezi hili au unaona kama unashindwa hakikisha kwanza unajilipa mwenyewe hapo utapata pesa ya kuweka akiba ya ziada.
3. UMEKUWA MUONGEAJI SANA

Mara nyingi umekuwa mtu wa kuongea sana na sio kutenda hali hii imekuwa ikikupunguzia mwendo wa kuelekea kwenye mafanikio na kujikuta unaendelea kukosa pesa katika maisha yako.


Kama unataka kufanikiwa na kuona ndoto zako zinatimia hakikisha unakuwa sio mtu wa maneno, jifunze kuchukua hatua muhimu kwa kutenda. Tabia hii ya kuongea sana ndiyo inayosababisha uendelee kukosa pesa katika maisha yako kila wakati.
4. HUJAJIWEKEA VIANZIO VINGI VYA PESA

Umekuwa ukikosa pesa mara kwa mara kutokana na kukosa vianzio vingi vya pesa ambavyo vingekupatia pesa za kutosha na kukupa uhuru wa kifedha. 
Unapokuwa na vianzio vingi vya pesa vitakusaidia wewe kusimama imara hata pale mambo yako yanapokwenda vibaya. 
Unataka kuachana na hali hii ya kukosa pesa, tengeneza vianzio vingi vya pesa vitakavyokusaidia baadae kwenye maisha yako.
5. UNAFIKIRI SANA JUU YA KUSHINDWA

Mara nyingi umekuwa ukiwaza vizuizi vinavyokuzuia kufanikiwa badala ya kuchangamkia fursa zilizopo. Umekuwa ukiwaza sana nikiwekeza hapa itakuwaje? au nitapata hasara? Kutokana na mawazo haya ni ukweli usiopingika ni moja ya kitu ambacho kimekufanya uendelee kukosa pesa katika maisha yako.
6. HUNA ELIMU YA KUTOSHA KUHUSIANA NA MAMBO YA PESA

Kutokana na kukosa elimu hii muhimu kwako, imekufanya uendelee kukosa pesa za kutosha kila kukicha. 
Kumbuka hii ni elimu ambayo haifundishwi rasmi shuleni wala nyumbani lakini ni muhimu sana katika maisha yako kujifunza.


Jifunze juu ya mzunguko mzima wa pesa unavyofanya kazi na suala zima la ujasiriamali na masoko.
7. UNAFANYA KAZI SANA KWA AJILI YA PESA

Hii ni sababu kubwa sana inayokufanya kila siku uendelee kukosa pesa. Maisha yako yanazidi kuwa magumu kila siku kwa sababu unafanya kazi kwa ajili ya pesa na matokeo yake unajikuta pesa inakufanya kuwa mtumwa kila siku.


Jifunze kutenda mambo yako kwa ubora wa juu na kwa viwango pesa zitakuja zenyewe. Kama unafanya biashara fanya kwa ufanisi na ubunifu wa hali ya juu, wateja watakuja wenyewe na utapata pesa za kutosha.


Acha kabisa tabia ya kuitumikia na kuifukuza pesa katika maisha yako. Na kama utaendelea kufukuza pesa, utashangaa katika maisha yako utakuwa mtu wa kukosa pesa kila siku.
Unaweza ukabadili na kufanya maisha yako vyovyote vile unavyotaka yawe kama tu utaamua, hizo ndizo sababu muhimu zinazokufanya uendelee kukosa pesa katika maisha yako.

No comments:

Post a Comment