Saturday, 30 November 2013

BAVICHA YAMPONDA MWENYEKITI MBOWE


3Taarifa yake nasema ‘Mimi Patrick Y.Joseph ni mwanachama na kiongozi wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA ninayeshikilia nyadhifa mbalimbali, Chama chetu kimekuwa na tabia ya kuingia kwenye migogoro kila panapokaribia chaguzi mbali mbali za ndani ya chama, migogoro hii hupelekea mpaka kuchafuana na kutukanana miongoni mwetu kiasi cha kuitana wahaini, wasaliti na wengine kuwaita wenzao wanatumika lengo likiwa ni kuwadhoofisha mbele ya wanachama na jamii kwa ujumla’

Tumeiona mifano mingi ya namna hii, wakati marehemu Chacha Zakayo Wangwe alipotangaza kugombea uenyekiti mgogoro wa namna hii ulijitokeza, aliitwa majina yote mpaka anapoteza uhai wake hakuwa akisemwa vizuri kwenye chama, hakuchafuliwa na watu walio nje ya chama. Alichafuliwa na viongozi wenzie waliotofautiana msimamo.


Alipotangaza zitto kabwe kugombea uenyekiti hali ikawa hiyo hiyo, akaitwa msaliti, anatumika na mengineyo mengi, alipotangaza kujitoa kugombea akaachwa kidogo apumzike.

Tunakumbuka yaliyotokea wakati wa chaguzi za ubunge wa viti maalum, tunakumbuka pia chaguzi za mabaraza ya chama, wakati nagombea nafasi ya umakamo mwenyekiti wa vijana nako pia waliogombea uenyekiti waliitwa kila aina ya majina.

Kwa kifupi migogoro hii ni ya kutengenezwa ili kudhoofishana kuelekea chaguzi za ndani ya chama.
Hivi sasa tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa chama tumeshuhudia tena Zitto Kabwe na Dkt Kitila Mkumbo wakikutana na dhahama hiyo hiyo.


Hali hii si nzuri kuruhusu iendelee kushamiri ndani ya chama maana haikijengi chama zaidi ya yote inakibomoa tu.

KUHUSU MAAMUZI YA KAMATI KUU
Nikiwa kama mjumbe wa Baraza Kuu la chama ninayewakilisha wilaya ya Temeke, na nikiwa kama mjumbe wa Kamati Tendaji ya Baraza la vijana la Taifa (BAVICHA)


Nimefadhahishwa sana na uamuzi uliofikiwa na kamati kuu ya chama dhidi ya ndugu Zitto kabwe na Dkt. Kitila mkumbo.
Ukiachilia mbali kwamba kamati kuu haikuwa na mamlaka ya kikanuni wala kikatiba kufikia maamuzi iliyoyafikia na kuyatangaza kwa umma.


Lakini imeonyesha ni jinsi gani wametawaliwa na Chuki, Ghadhabu, Unafiki na Ubaguzi uliopitiliza.

Ni uamuzi ambao hauwezi kuungwa mkono na mwanachama yeyote mwenye akili timamu,kwa kuwa haukisaidii chama badala yake unapandikiza chuki miongoni mwa wanachama.
Uamuzi huu uliojawa na hofu kubwa ya kiuchaguzi, hofu ya madaraka na hofu ya kupoteza umarufu unapaswa kukemewa na kusababisha watu wenye akili timamu wajiulize mara mbili mbili kama ni sawa ama la.


Kwa mantiki hiyo basi, nikiwa kama mjumbe wa baraza kuu, ninatoa masikitiko yangu kwa kamati kuu kufanya kazi isiyowahusu tena bila kufuata hata kanuni wala Taratibu zozote za kinidhamu baina ya viongozi.

Ningependa umma utambue kuwa sikubaliani na uamuzi huu kwa kuwa haukidhi misingi ya kidemokrasia wala kufuata utawala wa sheria.

Haiingii akilini hata kidogo kwa chama kinachopanga mikakati mbali mbli ya kuhinda dola, kuwafukuza na kuwaogopa watu wanaopanga mikakati ya wao kushinda uchaguzi ndani ya chama.

Kama ni kweli kupanga mikakati ya uchaguzi ndani ya chama ni uhaini na usaliti, basi Operesheni zetu za chama ikiwemo M4C zenyewe zinapaswa kuwa uhaini uliopitiliza kwa kuwa nazo ni mikakati ya chama kushika dola.

MSIMAMO WANGU.

Ninamtaka mwenyekiti akishirikiana na watendaji wengine wa chama waitishe mkutano wa dharura wa baraza kuu ili tutolee maamuzi sahihi swala hili.

Ninataka pia pamoja na agenda zitakazojadiliwa,
(i). watueleze ni kwanini wameamua kusambaza waraka wanaozani unawadharirisha kina zitto na mkumbo badala yake waraka huo unakidharirisha chama kwa kuonyesha madhaifu ya mwenyekiti na katibu mkuu wa chama.


(ii). Ni kwanini tusiamini kwamba maamuzi haya yameathiriwa na hofu ya chaguzi za ndani ya chama .

(iii). Ni kitu gani kimeifanya sekretarieti ya kamati kuu itangaze ratiba ya uchaguzi mkuu wa ndani ya chama baada ya kuwachafua miongoni mwa watu waliotarajiwa kugombea nafasi mbali mbali mpaka kuwavua uanachama.

Ni vema sasa tu tukijenge chama chetu bila kufuata maswala ya ubaguzi wa kidini na kikabila ama kikanda.

Chama chetu kimekuwa kikishtakiwa sana kuhusiana na matatizo ya kidini na kikabila, lakini pia chama chetu kimekuwa kikiwatumia Zitto na Arfi kama ishara ya kutokuwa na udini ndani ya chama, sasa inawezekanaje kuwatimua na kuwaita wasaliti watu ambao mmekuwa mkijivunia.

Mwisho ninapenda kusema kuwa huu ni msimamo wangu na kwamba sipo tayari kuburuzwa wala kuruhusu kuona tunaendelea kuibomoa demokrasia tunayoitangaza kila kukicha.

Nitaendelea kuwa mwanachama mtiifu wa chama changu, na kukishauri namna bora ya kuendeleza demokrasia ndani ya vikao na sita ogopa kueleza maoni yangu kwa Watanzania.


Joseph Y. Patrick
Mwenyekiti wa chadema wilaya/jimbo Temeke
Mwenyekiti BAVICHA mkoa wa Temeke
Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema Taifa
Mjumbe wa mkutano  mkuu wa Chadema Taifa

No comments:

Post a Comment