Tuesday, 26 August 2014

THELUTHI MBILI ZAKOSEKANA KAMATI MBILI

Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba,Samia Salum Suluhu.
Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samia Salum Suluhu, amesema kamati namba saba na nane zimeshindwa kupata theluthi mbili, kutokana na uchache wa wajumbe kutoka Zanzibar.
Alisema, tangu mwanzo kamati hizo zimeshindwa kupata theluthi mbili kutokana na maumbile yao baada ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wanachi  kutoka nje.

“Kamati hizo kwa maumbile yao, zina wajumbe wengi kutoka Bara na wachache kutoka Zanzibar.  Kila wanavyopigania kura, hawawezi kufikia theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar,” alisema Suluhu.

Kwa mujibu wa Suluhu, kwa mazingira hayo watajionyesha kwa jinsi walivyopiga na kwamba, kwa jinsi  Wazanzibari  walivyo wachache kwenye Bunge, ndiyo maana baadhi ya kamati zilipata wajumbe wachache.

Alisema kati ya mambo manne waliyopewa kuyashughulikia baada ya kuleta mvutano mkali kwenye kamati, wamemaliza suala la Mahakama ya Kadhi na uraia pacha na kwamba maoni na mapendekezo yao yamepelekwa kwenye kamati ya uandishi ambayo italinganisha na mapendekezo ya kamati.

Alisema Jumamosi walijadili kwa pamoja suala la Kamati Fedha kati ya Zanzibar na Bara na Muundo wa Bunge.

Alisema wanaendelea kupokea maoni na kwamba licha ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kusema hatua ya sasa ni kujadili, lakini kanuni za Bunge hilo zinaruhusu kupokea maoni mapya.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment