Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi amejikuta katika wakati mgumu mbele ya Rais Jakaya Kikwete baada
ya kuzomewa hadi kukatisha hotuba yake akipingwa na wananchi pamoja na
madiwani wa CCM wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma alipokuwa akitetea
kuwapo kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).
Lukuvi alikumbana na mkasa huo wakati akijibu hoja
za Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM), David Malole ambaye alitaka CDA
ivunjwe akiituhumu kuwavunjia wananchi nyumba bila kuwatafutia mahali pa
kuishi.
Kuzomewa
Baada Malole kutoa madai hayo, Lukuvi ambaye ni
Mwenyekiti wa Bodi ya CDA alilazimika kupanda jukwaani ili asawazishe
kauli za mbunge huyo, jambo ambalo liliibua zogo na wananchi kuzomea.
Zomeazomea dhidi ya Lukuvi ilitawala katika
kipindi chote alichokuwa jukwaani huku viongozi wa chama wakihaha
kuwazuia wanachama na madiwani wa CCM wasizomee bila mafanikio.
Hali iliendelea kuwa mbaya kwa Lukuvi pale aliposema, “Mimi ni
mdau mkubwa wa CDA na ni kati ya watu ambao walishiriki kupeleka
maendeleo katika Mji wa Dodoma.”
Kauli hiyo ilisababisha madiwani pamoja na
wananchi kuanza upya kumzomea huku wakimtaka ashuke jukwaani kwa madai
kuwa hana cha kuwaeleza hadi wamwelewe.
Hali hiyo iliambatana na nyimbo zilizoanzishwa na
madiwani, “CCM.. shuka chini, CCM shuka chini” hali iliyomfanya Lukuvi
kushuka jukwaani.
Baadaye Rais Kikwete akizungumza na wakazi hao,
alitoa siku saba kwa viongozi wa mkoa kwa kushirikiana na mbunge kukaa
na kutatua mgogoro huo na aliahidi kukutana nao Septemba 8, mwaka huu.
Alisema migogoro haiwezi kutatuliwa katika mikutano ya hadhara, bali vikao vya kazi. Aliwataka kukutana kuangalia ni jinsi gani watamaliza mgogoro huo bila kuwa na fujo wala lawama.
No comments:
Post a Comment