Tuesday, 26 August 2014

MEYA WA CHADEMA ASUSIA MBIO ZA MWENGE

MEYA wa Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Japhary Michael kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amesusia kushiriki Mbio za Mwenge wa Uhuru katika manispaa anayoiongoza.

Kutokana na kitendo hicho, kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa, Bi.Rachel Kasanda, alidai kusikitishwa na hali hiyo akisema Michael hakuwatendea haki wananchi anaowaongoza.

"Mwenge huu si wa chama chochote cha siasa bali hii ni nembo ya Taifa, upo kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya wananchi," alisema.

Alisema pamoja Michael kushindwa kutoa ushirikiano, mbio za Mwenge huo zimezindua barabara ambayo ipo Mtaa wa Shahili anaoishi Meya huyo ambako ana nyumba na duka labiashara.

"Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi yake kutoshiriki katika mbio za Mwenge nchini tangu ulipowashwa Mei 2 mwaka huu na Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal Mjini Bukoba, mkoani Kagera," alisema.

Bi. Kasanda alisema, Meya huyo hakupaswa kususia Mwenge wa Uhuru ambao unaleta maendeleo kwa Watanzania na barabara iliyozinduliwa katika mtaa huo inatumika na watu wote bila kujali itikadi ya vyama vya siasa, rangi au dini.

Hata hivyo, Michael ambaye baada ya uzinduzi wa barabara hiyo alikuwepo dukani kwake, alisema amewakilishwa na madiwani watatu wa chama chake.

Alisema msafara wa Mwenge ulikuwa na madiwani wengine wa CHADEMA akiwamo Diwani wa Kata ya Kiusa, Stephen Ngasa hivyo hapakuwa na ulazima wa yeye kuwepo.

 Chanzo;Majira

No comments:

Post a Comment