Wednesday, 27 August 2014

PINDA ATAVUNJA MWIKO WA MAWAZIRI WAKUU?

Waziri Mkuu,Mizengo Pinda.
 
Uamuzi wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwakani unamuingiza kwenye orodha ya mawaziri wakuu wastaafu watano ambao walijitumbukiza katika kinyang’anyiro hicho, lakini hawakufanikiwa.
Jana magazeti mengi ya kila siku yaliandika habari kwamba Pinda ametangaza nia ya kuwania nafasi hiyo, ingawa yeye mwenyewe hakupatikana mbali na vyanzo vya ndani vya mkutano wake jijini Mwanza kusema kwamba kiongozi huyo ambaye amekalia kiti hicho tangu Februari, 2008 anautaka urais.

Kama Pinda hatimaye atafanikiwa kuteuliwa na chama chake na kisha kushinda urais, atakuwa amevunja mwiko wa watangulizi wake watano ambao walijaribu bila mafanikio.

Hata hivyo, kama Pinda naye atashindwa atakuwa ameongeza idadi na kuzidi kuthibitisha mwiko kuwa ukishakuwa Waziri Mkuu Tanzania ni vigumu kuufikia urais.

Mawaziri wakuu wastaafu wote mbali na Mwalimu Julius Nyerere aliyekamata kiti hicho kwa mwaka mmoja tangu 1961 hadi 1962, wengine wote kila walipojaribu kuwania urais ama walishindwa kwenye kura au majina yao yalikatwa na vikao vya chama tawala.

Wa kwanza kujaribu mara mbili na kushindwa ni John Malecela mwaka 1995 na 2005. Jina lake lilikatwa mara zote mbili.

Wa pili ni Jaji Joseph Warioba mwaka 1995. Jina lake liliishia ngazi ya Halmashauri Kuu  ya Taifa (NEC) baada ya kupata kura chache.

Wa tatu ni Cleopa Msuya mwaka 1995 ambaye alifika ngazi ya Mkutano Mkuu na kushindwa na wenzake wawili, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

Wa nne ni Dk. Salim Ahmed Salim aliyejaribu karata yake mwaka 2005 kama ilivyo kwa Msuya alifika ngazi ya Mkutano Mkuu sambamba na Jakaya Kikwete na Prof. Mark Mwandosya, lakini alipata kura chache nyuma ya Kikwete.

Wa tano ni Frederick Sumaye mwaka 2005 ambaye aliishia ngazi ya NEC kutokana na idadi ndogo ya kura.
Mawaziri wakuu Dk. Salim (1984-1985).Malecela (1990-1994). Msuya (1980-1983 na 1994-1995) Warioba (1985-1990). Sumaye (1995-2005).

MAONI KUHUU PINDA
Wadau mbalimbali  wametoa maoni tofauti kuhusiana na uamuzi wa Pinda baadhi wakisema anafaa na wengine wakisema hana sifa za kushika nafasi hiyo kubwa kuliko zote nchini.

Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, amemtaja Pinda kuwa ni miongoni mwa viongozi wachache wa CCM wanaoweza kufikiriwa na chama hicho kutokana na uadilifu, upeo katika mambo mbalimbali ikiwamo masuala ya ndani na nje ya nchi.

Alisema siyo kosa ndani ya CCM mwanachama kutangaza nia ya kugombea nafasi hiyo na kwamba Pinda na makada wengine waliotangulia kufanya hivyo wapo sahihi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema Pinda kama mwananchi na mwanachama wa CCM anao uhalali wa kutangaza nia yake na wala kwa kufanya hivyo hajalikoroga iwapo anajiamini anazo sifa mahususi za kuomba ridhaa ya chama chake.

Alisema kwa mtazamo wake kutokana na uadilifu wa Pinda na mtu ambaye amelelewa katika makuzi mazuri ikiwamo kukaa Ikulu kwa muda mrefu.

Alisema siyo dhambi kwa kuwa yupo madarakani na angetaka utulivu na kuona chama kinatulia, angesubiri muda muafaka mwaka ujao tungeelewa kwamba anataka Watanzania wajue mapema.

Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Ruaha-Iringa, Rwezaura Kaijage, alisema uamuzi wa Pinda unatakiwa uwasaidie Watanzania kujiweka tayari kwa ajili ya kuchambua pumba na mchele iwapo tunamhitaji kiongozi wa aina gani.

“Inabidi jumuiya ya Watanzania itazame uwezo wake na imtendee haki.Nafikiri tumepata pa kuanzia, tusubiri tuone CCM watafanya nini baada ya Pinda na Mwigulu Nchemba kutangaza nia ya kuwania Urais wakati chama chao kiliwafungia wengine kwa mwaka mmoja kujihusisha na siasa,” alisema Kaijage.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Kessy, alisema Pinda ana haki ya kutangaza azma yake kwa kuwa analindwa na uadilifu alionao ambao mpaka sasa haujatiliwa shaka na Watanzania wenzake na kwamba anayo nafasi ya kuungwa mkono.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Katavi, Dk. Prudencia Kikwembe, alisema iwapo Pinda ameamua kutangaza nia hiyo, Watanzania wako nyuma yake kutokana na rekodi aliyojiwekea katika kipindi chake uwaziri mkuu.

“Amejitokeza na wapiga kura wanamfahamu vizuri na lazima tuelewe kwamba Mungu ndiye anayetoa karama ya uongozi. Sisi kama wana CCM tuko tayari kumuunga mkono yule atakayepewa ridhaa na chama. Ingawa makundi yamejitokeza, lakini tuombe apatikane kiongozi mwadilifu na msikivu kwa watu wake,” alisema Dk. Kikwembe.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu, Kanisa Katoliki, Mwanza, Yuda Thaddeus Ruwai’chi, Pinda ana sifa za msingi.

Alitaja sifa hizo kuwa ni pamoja na uraia wa Tanzania na kutokuwa na historia ya matukio ya uhalifu kama vile vitendo vya uhaini.

Kuhusu uwezo wake katika kuongoza iwapo atagombea urais mwakani kupitia CCM,  Askofu Ruwai’chi, alisema, Waziri Mkuu, Pinda anazo sifa za kuongoza.

Alibainisha baadhi ya sifa hizo kuwa ni pamoja na kuwapo serikalini katika nyadhifa mbalimbali za kwa miaka mingi.

Naibu Spika, Job Ndugai, alisema nafasi ya urais kwa Pinda ni kubwa mno kutokana na kuhitaji maamuzi magumu  kuhusu mambo yanayoikabili nchi.

“Suala la utawala sio tu uadilifu, ili uwe Rais yapo mambo mengi ya kufanya, kwa Pinda bado hajawa na sifa  za kuwa Rais, ” alisema Ndugai.

Mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labour (TLP), Agustino Mrema,  alisema Pinda anaweza kuwa rais kwa kuwa hana makundi ndani ya chama chake na pia si mla rushwa.

William Simwali, Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Wilaya ya Mbeya Vijijini, alisema Pinda ni mpole sana kwa kazi ya urais itamsumbua sana ingawa ni mwadilifu.

Naye Kamishna wa NCCR-Mageuzi Mstaafu wa Mkoa wa Mbeya, Diamon Mwasampeta, alisema ingawa Pinda hana kashfa inayojulikana hadharani hadi sasa, y bado hatoshi kuwa rais kwa kuwa hata Bunge tu liliwahi kwa mara tatu kukusanya kura za kutokuwa na imani naye kwa kile kilichosemwa ni kushindwa kuchukua maamuzi kama msimamizi mkuu wa shughuli za serikali bungeni.

“Mfano, katika suala la mauaji ya albino, yeye alilia bungeni, lakini haitoshi, suala la unyanyasaji uliofanywa katika operesheni Tokomeza alishindwa kuwachukulia hatua mawaziri walio chini yake hadi pale Rais alipoingilia kati, huo ni udhaifu mkubwa sana, nadhani angepumzika tu kwani hawezi kabisa kwa nafasi hiyo,” alisema Mwasampeta.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (Teku) Mbeya, Dk. Stephen Mwakajumilo, alisema inda hanabudi kujipima kabla hajaamua kuchukua fomu kuwa ni kwa kiasi gani amekidhi matakwa ya wananchi alipokuwa katika nafasi ya uwaziri mkuu.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mbeya Mjini, Sambwee Shitambala, alisema Pinda anastahili kuwa rais kwa kuwa tayari amekuwa kiongozi mkubwa katika serikali na ni mwadilifu.

Mwanaharakati Jidawaya Kazamoyo wa jijini Mbeya, alisema kuwa nchi hii haihitaji kiongozi anayeshangaa mambo, kulalamika na kulialia kila wakati mambo ambayo yameonekana kufanywa dhahiri na Pinda.

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa umma(Chaumma) mkoani Dodoma, Kayumbo Kabutali, alisema Pinda anafaa kutokana na kuonekana anaweza kuwa rais kwa kuonyesha uchungu wa mauaji ya walemavu wa ngoz i(albino) na maendeleo ya watanzania kwa ujumla.

Aidha, alisema Pinda amesimamia vizuri zoezi la Kilimo Kwanza, hivyo akipata fursa ya kuwa rais ataweza kutekeleza na kufikia malengo.Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanataaluma katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udomasa),paul Loisulie, alisema Pinda wengi hawana mashaka na uadilifu wa Pinda pamoja na uzoefu.

“Ukizingatia kabahatika kukaa Ikulu awamu zote za Uongozi, Kwangu Mimi sifa wala si tatizo ila changamoto kubwa ni kile kiitwacho kete ndani ya chama Cha Mapinduzi kulingana na aina ya mtu atakayeweza kunadi chama ikashinda,” alisema Loisulie.

Mfanyabiashara ndogo ndogo wa mjini Dodoma, Zuhura Yusuph, alisema Pinda anafaa kuwa rais, lakini anakabiliwa na changamoto kubwa ya makundi ndani ya chama chake.

“Mimi binafsi Pinda sijawahi kumsikia anakabiliwa na tuhuma mbaya huyu ni muadilifu, yeye anahangaika tu aone Watanzania wanaondokana na umaskini kwa kutumia fursa zilizopo,” alisema.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Nicholaus Mgaya, alisema Pinda ametumia haki ya msingi  ya kikatiba.

“Kitendo cha Pinda cha kutangaza nia ya kutaka kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi ujao wa mwaka 2015, siyo cha kushangaza kwani ni haki ya kila Mtanzania mwenye akili timamu, ambaye hajawahi kushtakiwa kutangaza nia ya kuwania uongozi , kwa hiyo Pinda katimiza haki yake ya kikatiba,” alisema Mgaya.

Alifafanua kuwa, atakayeamua kuwa Pinda anafaa au la ni watanzania ambao watampigia kura baada ya kupita katika michakato ya kichama.Rais wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) Gratian Mukoba, alisema ni haki ya kila mtanzania kuwania nafasi anayoitaka kwa kama alivyoamua Pinda.

“Huwezi kusema kuwa kiongozi fulani anafaa ama laa, kwani  kila mtu anamitazamo yake juu ya kile alichokiamua na kukifanya hivyo nadhani tusiingilie sana huko tutaona itakavyokuwa,” alisema Mukoba.

Alichowahi kusema Pinda kuhusu urais soma ukurasa wa 22.
Mwissho
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment