Wednesday 27 August 2014

UGONJWA WA KISUKARI NIHATARI NA TISHIO KUBWA NCHINI

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, akiangalia kitabu chenye taarifa za ugonjwa wa kisukari baada ya kufungua mkutano wa pili wa wataalam wa ugonjwa wa kisukari kutoka mataifa mbalimbali Afrika na Ulaya wa Pan African Diabetic Foot Study Group. Katikati ni Rais wa Chama cha Utafiti Maradhi ya Kisukari Ulaya, Profesa Andrew Boulton na Mwenyekiti wa wa Pan African Diabetic Foot study Group, Dk. Zulfiqarali Abbas.
 
Serikali imesema kuna umuhimu wa kupima afya mara kwa mara ili kuepukana na maradhi kama kisukari ambayo hivi sasa yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku na kufikia milioni 1.8 hapa nchini.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, wakati akizungumza kwenye mkutano wa pili wa siku tatu wa Pan African Diabetic Foot study Group.

Alisema wagonjwa wa kisukari wamekuwa wakishambuliwa na vidonda miguuni hivyo kuna umuhimu kwa wagonjwa hao kwenda kupima mara kwa mara ili kupunguza athari.

Alisema licha ya dawa za ugonjwa wa kisukari kuwa za gharama kubwa, upatikanaji wake pia wa shida hivyo kuwasumbua watu wenye maradhi hayo.

Alisema serikali itajitahidi kuweka kliniki za kisukari katika hospitali za wilaya ili wagonjwa wasihangaike kwenda umbali mrefu kupata huduma katika hospitali za mikoa.

“Serikali imeutambua ugonjwa wa kisukari kama moja ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo wagonjwa wake wanapaswa kupewa dawa bure, nia ya dhati ipo ila fedha bado tatizo katika kutekeleza nia hiyo,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Pan African Diabetic Foot Study Group ambaye pia ni Mwenyekiti wa mradi wa miguu wa Step by Step,  Dk. Zulfiqarali Abbas, alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye mzigo mkubwa wa magonjwa wa kisukari na madhara ya ungonjwa wa kisukari kwenye miguu.

“Tanzania ina mzigo mkubwa wa magonjwa yasiyoambukiza, siyo tu kisukari, bali na matatizo yanayoambatana na ugonjwa huu kama vile vidonda vya kisukari miguuni, ambalo ongezeko lake haliwezi kufumbiwa macho,” alisema Dk. Abbas.

Dk. Abbas alisema wajumbe wa mkutano huo wanatoka nchi tisa nje ya bara la Africa, wajumbe ishirini na tisa kutoka nchi za Afrika na wajumbe kutoka mikoa ishirini na sita ya Tanzania.

Alisema lengo la mkutano huo wa siku tatu ni kutoa taarifa zilizopo kwa wakati huu kuhusiana na kinga na matibabu juu ya vidonda vya kisukari miguuni katika Afrika.

Alisema wasemaji tofauti ambao wapo kwenye Nyanja hii ya vidonda vya kisukari miguuni watawasilisha hotuba adilifu na kwamba mbali na hotuba hizo pia kutakuwa na maonyesho ya vitendo jinsi ya kuhudumia vidonda vya kisukari miguuni.

No comments:

Post a Comment